ASKARI AMUUA MWENZIE KWA RISASI 19 KISA WIVU WA MAPENZI


ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Praiveti Pascal Lipita (28), anayefanya kazi katika wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi cha 843 Nachingwea, mkoani Lindi, amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.

Lipita (28) anatuhumiwa kumuua askari mwenzake, Praiveti Baserisa Ulaya kwa kile kinachodaiwa kuwa wivu wa kimapenzi.

Mtuhumiwa huyo alifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa huo, Maria Batulaine, na kusomewa shtaka linalomkabili.

Mwanasheria wa Serikali, Abdulrahman Mohamed, alidai kuwa askari hao walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kwamba wivu ndio unaodaiwa kusababisha mauaji hayo.

Mwanasheria huyo wa serikali alidai kuwa mshtakiwa alifanya mauaji hayo Februari 10, mwaka huu, majira ya Saa 12;00 jioni wakiwa kambi ya Nang’ondo.

Alidai kuwa siku hiyo ya tukio, wakiwa kambini hapo, mshitakiwa akiwa na silaha, alimmiminia askari mwenzake risasi 19 kisha kuchakaza mwili wake na kumkatisha uhai.

“Baada ya kumpiga risasi moja na kuanguka chini, mshtakiwa aliendelea kummiminia zingine mwili wote na kumpotezea uhai wake,” alidai Mohamed.

Mwanasheria huyo alidai kuwa kutokana na kitendo hicho, mshtakiwa alifanya kosa chini ya kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo mwaka 2002.

Hata hivyo mshtakiwa hakutakiwa kukubali wala kukataa mashtaka yanayomkabili kwa kuwa mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi zinazohusu mauaji.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hayo, alipelekwa rumande na atafikishwa tena mahakamani Machi 2, mwaka huu, kesi itakapotajwa

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.