KUSUKUMWA NA UPENDO 1




Hadithi=> KUSUKUMWA NA UPENDO
Sehemu ya : 1 ***msituni
 Tulikuwa pamoja na Bobby tulipokutana na Ayaboquina, kiongozi wa Wamotilone, kabila moja la wahindi wekundu. Alikuwa peke yake msituni akifanya kazi ya kufyeka msituni. Vichipukizi vya migomba vyenye rangi ya kijani na vipuko vya “Yukka” [aina Fulani ya mimea] vilionekana ardhini. Palikuwa mahali pa kutosha kwa mifugo kulishwa pale kwenye kiwanja chenye eka hamsini na tano. Tulipokuwa tukizungumza na Ayaboquina juu ya maendeleo ambayo wahindi wekundu walifanya, tulisikia sauti ya mashua iliyoendeshwa chini mtoni. Ilikuwa karibu zaidi ya ukingo, kwa hiyo hatukuweza kuiona lakini tulisikia jinsi ilivyovutika. Kwa kawaida huchukua kitambo kidogo kabla ya kufika mahali tulipokaa, lakini kwa ghafla mtu mwenye uso mweusi alitokea.
 “Habari za mchana,” alisema kwa sauti kali katika lugha ya kihispania.
 Alikuwa amekasirika na hakutaka kusubiri mpaka nimalize mazungumzo na Ayaboquina. Nilifahamu ya kuwa alikuwa Humberto Abril, mmoja wa wageni watoro waliokuja kukaa hapa. Nilijua ya kwamba alikuwa na hasira na kwamba aliwatia hofu Wamotilone. Sasa ilionekana wazi kuwa amekasirika kweli.
Nilipomaliza mazungumzo yangu na Ayaboquina, nilimsalimu nikisema, “Habari za mchana Humberto”! Jasho lilitoka kwenye uso wake ambao ulikuwa na umbo la kuogofya.
 “Nimekuja kukuambia kuondoka nchi hii”, akasema. Nchi hii ni yangu. Mimi ni mkoloni wa Colombia. Nina haki kudai nchi hii kwa ajili ya kufanya ukoloni wangu na ninaitaka nchi hii. Sasa mnaweza kuondoka….”
 Alipokuwa akisema nami Bobby alimdakiza. “Na mimi nina neno la kukuambia,” alisema polepole kwa utulivu, lakini kwa nguvu. Nchi hii ni yetu, imekuwa nchi yetu daima. Tumewapa ninyi nchi za kutosha. Miezi sita iliyopita tuliwapa nchi Fulani kwa sababu ya madai yenu, na sasa mmefanya nini? mmeuza nchi ile na sasa mnadai zaidi. Lakini hatutakubali kuwapa nchi zaidi. Sisi tunataka kuilinda nchi ambayo ni yetu.
 Hoja yake ilikuwa fupi lakini Humberto alianza kutetemeka. Misuli ya shingo yake ilikuwa kama kamba za chuma. Uso wake ulianza kuwa mwekundu kabisa. Alimshika bobby mabegani na kupaza sauti: “Hii ni nchi yangu,” mtu mwingine yeyote lazima aondoke. Kisha alimwachia Bobby akasimama huku akitetemeka. Hofu kubwa ilinishika mgongoni kama barafu kali. Lakini boby alikuwa na matumaini.
 “Umekosa! Nchi hii si nchi  yako, na haitakuwa nchi yako,” alisema polepole.
 “Nyamaza”, Humberto akapiga yowe. “Nyamaza wewe mhindi mwekundu mchafu, nyamaza.” Mate yalitoka mdomoni mwake na yalifanya kama madoa madogo katika uso wake mwekundu. Aliweka kidole chake cha shahada  juu ya kidole gumba cha mkono wake wa kuume ili kufanya kama msalaba. Aliendelea kuvishikilia vidole katika hali ya msalaba. Alikodoa macho huku mikono ikitetemeka, na hatimaye hakuweza kuvishikilia vidole vyake, akavibusu.
 “Ninaapa kwa jina la Mungu” alisema huku akivibusu vidole vyake tena na kutema mate chini. Kwa watakatifu! Akatema mate tena. Kichwa chake kikashtuka, kwa bikira mariamu! Akatema mate mara ya tatu. Na kwa msalaba! Akatema mate. Alitutazama akainua kidole chake cha shahada na kidole gumba akavitia mdomoni na kuvibusu. Sauti yake ilikuwa ya kukoroma. “Nitawaua”, akapiga yowe tena, “Ninaapa kwa msalaba huu nitawaua.”
 Aligeuka na kushuka kando akaenda hadi ukingoni. Tulimfuata kwa kumtazama hadi alipotoweka katika upeo wa macho yetu. Wakati anaondoka shingo yake ilikuwa bado nyekundu na misuli na mishipa yake  ilionekana kama nyuzi za gitaa.
 Tulikaa kimya mpaka tuliposikia akiwasha mashua na kutoweka kwa mbali. Nilitetemeka. Bobby, anafanya hivyo! Atatuua. Ninajisikia hivyo kwamba amedhamiria kabisa. Unasema kweli Bruchko. Tufanye nini sasa? Ayaboquina, Bobby na mimi tulikata shauri kujihadhari naye.
___ITAENDELEA___

Toa maoni yako ili tuzidi kuwa pamoja zaidi

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.