KUSUKUMWA NA UPENDO 5



Hadithi=> KUSUKUMWA NA UPENDO
Sehemu ya : 5 ***Nani ni Mungu wangu?
 “Nani ni Mungu wangu?” Niliuliza nilipokuwa na umri wa miaka kumi na mine. “Yeye ni nani?”
 Hakukuwa na mtu wa kunijibu. Ng’ambo ya kiwanja cha shule ya sekondari niliweza kusikia sauti za vishindo na filimbi kutoka mazoezi ya mchezo wa mpira. Mara elfu nilipenda niwe hodari wa kutosha katika michezo ili nishirikishwe. Lakini mawazo yangu yalifikiri juu ya jambo jingine pia, juu ya jambo moja ambalo lilinisumbua siku nyingi.
 “Nani ni Mungu wangu”, nilijiuliza tena. Kuna Mungu wa Kilutheri ambaye tunazungumza habari zake kanisani. Tena kuna Mungu tunayesoma habari zake shuleni, Mungu wa wakristo wa makanisa yote. Na kuna Mungu ninayesoma habari zake katika Biblia. Lakini katika hao wote, yupi ni Mungu wangu? Sikupata jibu lolote kutoka anga baridi la Minnesota. Nilianza kutembea kuelekea nyumbani.
 Ilionekana kwamba hakuna mtu yeyote mwenye kunipa jibu. Jumapili iliyopita nilijipa moyo wa ujasiri nuikamuuliza mwalimu wangu wa shule ya jumapili. Na yeye alipasua kicheko!
 “Je, hukutoa ahadi za kipaimara?”
 Nilifahamu mambo yote juu ya kipaimara. Nilipokuwa ninajifunza katika mafunzo yanayofundishwa kabla ya kupata kipaimara nilijifunza kinadharia tu, juu ya elimu ya Mungu. Lakini nilikuwa na hamu yakumjua Mungu.
 Baba yangu hakutaka niwe na mawazo ya namna hiyo. Nilikuwa sijamwuliza, lakini nilijua angesema nini kama ningemwuliza. Angenitazama kwa macho yake ya buluu yaliyo wazi na kuniambia kwamba ninapoteza muda wake na wangu. Labda nilifanya hivyo kweli. Ilionekana haikueleweka vizuri kwangu kwamba kuna Mungu mwingine zaidi ya Mungu mkali wa Kilutheri. Kila nilipowaza nilimwogopa. Baridi hii ya theluji inayoniumiza usoni ni hewa yake, nilifikiri. Niliyapiga teke majani makavu yaliyokuwa kando ya barabara. Asubuhi maeneo yote yalikuwa meupe kama theluji. Hata wakati huu kulikuwa na masalia machache ya theluji.
 Kwanini nilizaliwa? Mimi ni mtu dhaifu mno….. sikuweza kuona vizuri isipokuwa vitu vilivyo karibu…..   sikuwa hodari. Sikuweza kucheza mpira vizuri. Walipopiga mpira upande wangu ulinigonga na walicheka…
 Niliweza kuuona uso wa Kent Lange wenye madoa mengi na nywele nyeusi zilizoviringana akinicheka sana. Alikuwa ni rafiki yangu sana. Niliona baridi na uzito tumboni kama nimemeza barafu kwa haraka. Kwanini nilichukulia maanani kila jambo? Huo ulikuwa ni mchezo tu. Nitakapofika nyumbani, nilifikiri, nitakusanya vitabu vyangu. Na matatizo yote nitayasahau.
 Nilipenda kuvitandaza vitabu kitandani – vitabu vya lugha mbalimbali. Siku mbili zilizopita, kila jioni nilijizoeza Kigriki kwa njia ya kusoma Biblia. Nilikuwa na Biblia kubwa yenye jalada la ngozi. Ilichapwa na kutungwa vizuri sana na nilipenda kupekua kurasa zake. Miaka mingi nilisoma Biblia, zaidi agano la kale. Sasa nilipoanza kujifunza Kigiriki nilivutiwa sana kusoma agano jipya.
 Lakini hata hivyo bado nilivutiwa sana kusoma agano la kale. Nilipendezwa sana na habari za kihistoria zilizoambatana na mapigano. Mara nyingi siku ya jumapili jioni nilisoma sura nyingi.
 Kulikuwa na tofauti kuhusu ujumbe wa manabii. Waliniogofya mara nyingi hata niliweza kufunga Biblia na kuiacha imefunikwa na mpaka nilifikia kiasi cha kuamini kwamba kitabu kile kilikuwa kitabu cha ndoto tu si kitabu cha unabii wa kweli kabisa.
 Siku ya hukumu ya Mungu ilikuwa rahisi kuifahamu. Ardhi itafunguka na watu watapelekwa chini jehanamu kwenye moto wa milele. Yesu atakuja mawinguni pamoja na mwaliko mkuu wa malaika na upanga mkononi mwake ili kuiharibu dunia na vyote vilivyomo kwa sababu ya dhambi.
 Niliogopa kufikiri juu ya Mungu. Mara kwa mara niliposhikwa na hasira nilijiona jinsi nilivyo mwenye dhambi na ndipo misuli ya tumbo langu ilipokazika. Hata hivyo sikuacha bali niliendelea kupigana na kutukana ingawa niliona hofu wakati wote. Baadaye nilifikiri, oh! Mungu wangu nitahukumiwa. Nilihuzunika, lakini ndani ya moyo wangu nilijua ya kwamba nitafanya mabaya tena.
____ITAENDELEA____

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.