MUSEVENI ATOA YA MOYONI KUHUSU SHAMBULIO LA LIBYA


RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amesema haikupasa nchi za Afrika ziruhusu nchi za Magharibi ziishambulie kijeshi Libya na kupelekea kuuawa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi.
Museveni, ambaye yuko nchini Uingereza alikohudhuria mkutano wa uwekezaji kati ya Afrika na Uingereza, aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa nchi za Afrika zilipaswa kuingilia kati nchini Libya na kwamba japokuwa zilijaribu kufanya hivyo kidiplomasia, lakini zingeweza pia kuingilia kijeshi.
Akizungumza kwa hasira, Museveni alisema laiti kama Afrika ingejiandaa vya kutosha, madola ya kigeni yasingeishambulia Libya na kumuua Gaddafi.
“Afrika ingeweza kuingilia kati na kutoa funzo kwa watu hao,” alisisitiza Museveni.
Aidha Museveni alisikitikia kifo cha Gaddafi, akikielezea kuwa ni matokeo ya Waafrika kushindwa kumlinda “mwana wao”.
Alifafanua kuwa Libya ni nchi ya Afrika ambayo ilishambuliwa na madola ya kigeni, hivyo nchi za bara hilo zilipaswa kuingilia kati. 
Katika mahojiano hayo na BBC, Museveni alisema Afrika haikupigana kuisaidia Libya kwa sababu shambulio dhidi ya nchi hiyo lilifanywa kwa kushtukiza.
Alifafanua kuwa hata yeye mwenyewe hakuweza kuamini kama kuna mtu anayeweza kuwa ‘mpumbavu’ kiasi cha kuishambulia nchi ya Kiafrika namna ile.
Aidha, Museveni alisema nchi za Afrika hazihitaji uingiliaji wa madola ya kigeni kutatua masuala yao ya ndani na akaongeza kuwa zinahitaji kuungana na kuongea “lugha moja” na kuweza kumshinda yeyote atakayejaribu kuwashambulia watu wao.
Alisema anaamini Afrika iliyoungana inao uwezo wa kuyashinda madola yoyote makubwa ya Magharibi yatakayojaribu kulivamia bara hilo, akikumbusha jinsi Afrika ilivyoweza kuwashinda na kuwatimua Wareno pamoja na makaburu waliokuwa wakisaidiwa na kuungwa mkono na madola hayo.

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.