MEYA WA ILALA AMEWATAKA WANAWAKE KUJIKITA KATIKA UWEKEZAJI


MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto amewataka wanawake wa halmashauri hiyo kujikita katika uwekezaji ili kujikwamua kwenye hali ngumu na kukuza uchumi wa nchi.
Hayo aliyasema jana Dar es Salaam, wakati akifunga mafunzo ya wanawake na vijana wajasiriamali wa Kata ya Gongo la mboto yalioandaliwa na Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo.
“Napenda kumshukuru Mwenyekiti wa Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo, Neema Mchau, kwa juhudi zake za kuisaidia Serikali, hasa wilayani Ilala kwani amewainua wanawake katika shughuli za uzalishaji, amewapatia ujuzi, sasa wanamiliki viwanda vyao,” alisema Kumbilamboto.
Alisema sasa ni wakati wa wanawake kusimama imara katika viwanda vidogo vidogo ambavyo vinazalisha bidhaa na kuzitangaza katika masoko ya ndani na nje.
Kumbilamoto alisema Serikali mwaka huu inakabidhiwa soko la kisasa la Kisutu ambalo ujenzi wake umegharimu Sh bilioni 13, litakapoanza kutumika soko hilo watawekwa wafanyabiashara wa awali na nafasi za wafanyabiashara 700.
Pia ameitaka taasisi hiyo na wafanyabiashara kuchangamkia fursa kwani soko hilo litakuwa la kisasa na watalii watafikia hapo na ndio mradi mkubwa wa soko la kipekee Ilala.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatoa mikopo ambayo haina riba kupitia halmashauri kwa vikundi vinavyotambulika, hivyo wakopaji wakope fedha hizo na wakumbuke marejesho ili wengine nao waweze kukopa.

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.