MOTO UNAWAKA KINANA, MAKAMBA WAJIVUA UANACHAMA CCM
MAKATIBU wakuu wastaafu wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, wamejivua uanachama wa chama hicho.
Habari zilizotufikia zinasema Kinana na Makamba walijiondoa rasmi CCM kwa maandishi. Barua zao, kila mmoja na ya kwake, zilifikishwa ofisini kwa Katibu Mkuu wa CCM tarehe 7 Februari 2020.
Chanzo kinachoaminika kutoka CCM Makao Makuu kimesema: “Barua zao zimefika kwa nyakati tofauti, zimepokelewa. Lakini inaonekana kama walikuwa wameziandika muda mrefu baada ya kushauriana, maana zinafanana na zimewasilishwa siku moja. Taarifa hizi zilipofikishwa kwa Mzee (Rais John Magufuli) zilimvuruga kwa kweli.”
Kwa mujibu wa chanzo hicho, ambacho hakitatajwa hapa, Rais Magufuli, baada ya kupokea ujumbe wa Kinana na Makamba kujivua uanachama, aliwaomba wazee wawili waandamizi – Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Spika Mstaafu Pius Msekwa – wamsaidie kuzungumza na akina Kinana ili kuwashawishi wabadili msimamo wao.
Hata hivyo, Kinana na Makamba wamegoma kusikiliza ushawishi wa mtu yeyote. Katika barua zao za kujiondoa CCM, kwa mujibu wa chanzo chetu, Kinana na Makamba waliambatanisha pia kadi zao za uanachama.
“Tayari wameturudishia kadi zetu, maana yake wao si wanachama wetu tena,” kimesema chanzo hicho.
Kinana na Makamba ni miongoni mwa makatibu wakuu wanaoheshimika katika CCM, wenye ushawishi, na ambao wametumikia nchi katika nyadhifa mbalimbali kuanzia jeshini hadi serikalini na kwenye chama.
Siku ambayo walikabidhi barua na kadi zao na kutangaza rasmi kujiondoa CCM, ndiyo siku walipotarajiwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya CCM iliyoagizwa na Rais Magufuli katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ili wajieleze kuhusu waraka walioanidika kwa Baraza la Wazee la chama hicho wakilalamikia kubezwa na kudhalilishwa na mhuni mmoja anayetumia jina la rais kudhihaki na kushambulia wakosoaji wa rais na serikali.
Mbali na Kinana na Makamba, mwingine aliyeitwa kuhojiwa na kamati hiyo ni Bernard Membe, waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambaye aliunga mkono waraka wa wazee hao, na pia alidukuliwa akizungumza katika simu mambo ambayo hayakumfurahisha Rais Magufuli.
Yeye alikutana na kamati hiyo Mjini Dodoma Ijumaa tarehe 7, Februari 2020; na baada ya mahojiano alionekana mwenye kujiamini na mwenye furaha.
Mmoja wa wajumbe walioshiriki mahojiano hayo amezungumza kwa sharti la kutotajwa, akisema: “Tulijuta kumuita Membe. Kuna maswali amehoji na masuala amezungumza nasi hadi tukahisi yeye ndiye anayetuhoji. Ukweli ni kwamba chama chetu kinahitaji mabadiliko makubwa ya kimsingi, maana kuna shida mahali. Bwana mkubwa anatupelekesha, na watu jasiri wa kumwambia ukweli hawapo, tunaishia kuagizwa tu, hata kutenda mambo yaliyo kinyume cha misingi ya CCM. Membe ametukumbusha yote haya. Kwa kweli, sijui kinachofuata.”
Kwa Kinana na Makamba kujivua uanachama na kugoma kuhojiwa, wamewaza hatua mbili mbele ya Magufuli. Chama hakiwezi kuwahoji kwa kuwa wao hawafungwi tena na nidhamu wala maadili ya CCM kwa kuwa si wanachama CCM.
Ingawa barua zao zilipelekewa kimya kimya, na uongozi wa juu wa CCM umekuwa unahangaika kuzuia taarifa hizi kuvuja, zilivuja mapema mno; na kitendo chao cha kutofika mbele ya kamati kuhojiwa kimezua maswali na mjadala mpana ndani na nje ya CCM.
Profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema: “Tusishangae sasa kusikia siku moja Kinana au Makamba wametiwa mbaroni na wanashitakiwa kwa utakatishaji fedha, maana hii ndiyo fimbo mpya ambayo inatumika kuumiza wanaotofautiana na watawala. Lakini iwapo watashitakiwa umma utajua kuwa sababu hasa si uhalifu wao bali ni hii barua yao na uamuzi wao.”
Kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM amesema: “Kiukweli, Mzee Kinana na Mzee Makamba hawana cha kupoteza. Nadhani sisi ndio tuna cha kupoteza, maana ukisoma waraka unaowasababishia haya yote utagundua kuwa wao ni watetezi wa misingi ya chama chetu. Wanachotetea ndicho wana CCM wote tunapaswa kutetea, lakini sasa tofauti iliyopo kati yetu na wao ni kwamba wao wameonyesha ujasiri ambao sisi hatuna. Wengi wetu tumebaki kutii maagizo ya bwana mkubwa, huku chama kinaporomoka!”
No comments