MWANAJESHI NCHINI THAILAND AFYATUA RISASI HOVYO NA KUUA


Mwanajeshi mmoja nchini Thailand amewashambulia kwa kuwafyatulia risasi watu kadhaa na kuua idadi "kubwa" ya watu.

Tukio hilo limetokea katika mji wa Nakhon Ratchasima pia ukijulikana kama Korat kaskazini mashariki mwa jiji la Bangkok.

Msemaji wa wizara ya ulinzi nchini humo amesema kuwa mwanajeshi huyo, Jakraphanth Thomma, alimshambulia mkuu wake kwanza kabla ya kuanza kufyatua risasi katika kambi ya kijeshi, hekalu la Buddha pamoja na kituo cha ununuzi.

Mamlaka za ulinzi na usalama zimezingira na kukifunga kituo hicho cha ununuzi ili kujaribu kumkamata mtuhumiwa, ambaye inasemekana bado yumo ndani ya jengo hilo. Polisi wamewaonya watu kujifungia ndani ya nyumba zao.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa watu wasiopungua 12 wameuawa katika shambulizi hilo.

Jarida la Bangkok liliripoti kwamba mtuhumiwa huyo, ambaye ametajwa kuwa na umri wa miaka 32, alikuwa amechukua baadhi ya watu kama mateka ndani ya jengo hilo, ingawa bado haijathibitishwa rasmi. Risasi zaidi zimeripotiwa kusikika ndani ya jengo hilo.

Nia na madhumuni ya mtuhumiwa kufanya shambulizi hilo bado haijajulikana wazi.

Hata hivyo, aliweka katika kurasa zake za mitandao ya kijamii matukio ya wakati alipokuwa akitekeleza shambulio hilo, na ujumbe mmoja katika ukurasa wake wa Facebook akiuliza ikiwa inampasa kujisalimisha.

Hapo awali alikuwa ameweka picha ya bastola iliyo na seti tatu za risasi, pamoja na maneno: "Ni wakati wa kufurahi" na ujumbe mwingine ukisomeka "hakuna mtu anayeweza kuzuia kifo".

Ukurasa wake wa Facebook sasa umefungiwa.

Jarida la Bangkok limesema kamanda ambaye ni marehemu ametambulika kama Kanali Anantharot Krasae, na kwamba mwanamke wa miaka 63 na askari mwingine waliuawa katika kambi ya jeshi.

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.