KOCHA AFUNGIWA KWA KOSA LA KUVUA SURUALI

SHIRIKISHO la Mpira wa miguu Zanzibar (ZFF) limemfungia miezi sita na kumpiga faini ya Sh 500000 kocha wa timu ya Miembeni Suleiman Mohamed kwa kitendo cha utovu wa nidhamu.

Juzi wakati timu yake ikicheza na timu ya Taifa Jang’ombe katika Uwanja wa Amaan, mchezo wa ligi daraja la kwanza kanda ya Unguja baada ya timu yake kushinda bao 1-0, kocha huyo alishangilia na kushusha suruali chini na kubaki na nguo ya ndani mbele ya mashabiki.

Kwa mujibu wa barua ya adhabu hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Kamati ya Mashindano ya ZFF Hussein Ahmada, wametoa adhabu hiyo kwa mujibu kifungu namba 31 cha kanuni ya kuendesha mashindano hayo.

Hussein alisema kocha huyo atatakiwa kulipa faini hiyo ndani ya kipindi anachotumikia adhabu hiyo na akishindwa kulipa faini adhabu itaendelea mara mbili.

“Tumesikia kabla ya mchezo huo kocha huyo aligombana na mashabiki lakini sisi adhabu tuliyoitoa ni kufanya kitendo hicho cha utovu wa nidhamu ambacho kimezagaa katika mitandao ya kijamii”, alisema Ahmada

. Pia Shirikisho hilo limeipiga faini ya Sh 100,000 timu ya Miembeni kwa kushindwa kumdhibiti kocha wao wakati akifanya vitendo hivyo na kusema vitendo vilivyofanywa na kocha huyo havikubaliki katika soka na hata mila na tamaduni za Kizanzibar.

Aidha ZFF imewataka viongozi wa timu hususani benchi la ufundi na mashabiki kuacha tabia ya utovu wa nidhamu pale timu zao zinaposhinda au kufungwa badala yake wazingatie kanuni za mashindano.

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.