KUSUKUMWA NA UPENDO 6



Hadithi=> KUSUKUMWA NA UPENDO
Sehemu ya : 6 ***Nani ni Mungu wangu?
 Agano jipya lilionekana kuwa tofauti. Kwa muda wa siku mbili kila jioni nilisoma injili ya Yohana. Nilishindwa kuelewa, Yesu alionekana tofauti kabisa na jinsi nilivyokuwa ninaamini. Au labda nimechanganya Yesu na Mungu huyu ambaye nilimwogopa? Kila mahali alipokwenda, Yesu alibadilisha maisha ya watu wengi. Na kila wakati walibadilishwa kuwa watu wema zaidi.
 Nilifikiri juu ya darasa langu la shule ya jumapili. Kila mvulana wa darasa hilo nilimfahamu. Nilikwenda kanisani pamoja nao kila mara. Lakini hawakubadilika hata kidogo. Hakuna hata mmoja wetu aliyebadilika.
 Kwa kweli yalikuwa mazungumzo mengi juu ya mabadiliko. Mchungaji alituambia, lazima mbadilishwe kwa sababu Mungu atahukumu dunia hii pamoja na watu wenya dhambi. Lazima mtakuwa watakatifu kama Mungu alivyo mtakatifu. Hilo ni agizo lake kwenu. Kupungukiwa na ukamilifu wake ni kupungukiwa na umilele wake.
 Hukumu iliniogofya. Mara nyingi Kent alikuja nyumbani kwangu jumamosi na tulizungumza juu ya habari za hofu kuu na filamu ambazo tulikuwa tumeona. Tulijaribu kuogofyana na tulichekelea na kuficha vichwa vyetu chini ya mito ya vitanda. Tuliifurahia hali ya hofu. Lakini tuliendelea kuzungumza juu ya hukumu ya Mungu na jehanamu iwakayo moto.
 Baadaye tulikaa kimya. Tulijua kwamba habari hii haikuwa uvumbuzi na mwongozo wa mtengeneza filamu au mwandikaji wa hadithi. Jambo hili lilikuwa ni jambo la kweli. Na lilikuwa ni jambo ambalo litatokea.
 Mama alikuwa akitayarisha chakula jikoni niliporudi nyumbani. Nilisikia baridi kwa sababu ya upepo mkali. Nilivua koti langu na kulitundika kisha nikaenda hadi jikoni huku nikisugua mikono yangu. Niliusukuma nyuma mmoja wa ushungi wake akanitazama.
 “Habari za shuleni leo, Bruce?”
“Njema tu”, nilijibu, “Baba yuko wapi?”
 Aliinamisha uso na kutazama chini. Ndugu yako na baba yako wamegombana. Yuko chumbani mwake.
 Kwa ghafla nilijisikia kuchoka sana saa ile! Kila mara kulikuwa na watu waliogombana katika nyumba yetu. Ilionekana njema zaidi wakati ambao hatukuzungumza.
 Nilipanda ngazi hadi chumbani kwangu. Ngazi zilionekana zimesuguliwa na kuwa safi ziking’aa kwa ile rangi nyekundu. Niliipenda rangi ile. Kila kitu kilitengenezwa vizuri na kilikuwa safi na cha kupendeza. Kwanini hata sisi tusiwe hivyo?
 Mtu angetuona angeweza kuamini kwamba mambo yote yanakwenda sawasawa. Mama yangu alikuwa Mswidishi mwenye uso mzuri sana, mkamilifu kama sanamu. Hakuna hata mmoja wa rafiki zangu ambaye alikuwa na mama mzuri kama mimi. Na baba yangu alikuwa mwenye sura nzuri pia, taya kubwa na nywele nyeusi ambazo kila wakati zilionekana kama zimechanwa sasa hivi. Lakini ni mara chache tulipatana.
 Niliingia chumbani mwangu nikaweka vitabu vyangu vya shulE. Hatimaye nilichukua vitabu vingine nikaviweka kitandani. Nilikuwa Biblia ya kiingereza, agano jipya la Kigiriki na vitabu vingine vya kunisaidia kufahamu Kigiriki.
 Niliunyosha mwili wangu mwembamba kitandani. Miguu yangu ilining’inia kiasi Fulani. Vitabu vilifanya duara kandokando yangu. Hali kama hiyo ilinifanya nijisikie niko nyumbani. Lo! Nilistarehe. Nilisoma mpaka jioni. Chakula kilipokuwa tayari, mama aliniita. Niliteremka chini nikakaa pamoja na jamaa yangu iliyokuwa kimya huku nikitafakari juu ya yale niliyoyasoma.
 Baba yangu aligundua ya kwamba sikusema neno. “Kwanini hutaki kutupa habari yoyote?” akauliza. Alizungumza kwa utaratibu sana.
 “Nilikuwa nafikiri juu ya mambo mengine baba”, nilisema. “Mambo gani?” Nilimtazama mama yangu, maana nilitaka nikwepe kujibu.
 Baba akasema, “Bruce, usimtazame mama yako ni mimi ninayekusemesha.” Nililazimishwa kujaribu kueleza. Nikasema kwamba nilikuwa najisomea Agano jipya na kwamba sikuweza kuelewa vizuri.
 “Ni wazi kwamba huwezi”, Baba akasema. “Maneno haya yaliandikwa miaka elfu mbili iliyopita. Huwezi kufikiri kuwa yana maana leo”
 Chakula kilinikwama kooni. Nilichoka kumsikia baba akizungumza maneno yale yale. Yeye anajua nini juu ya mambo haya? Nilijiuliza huku nikitazama ndani ya sahani yangu. Ingekuwa rahisi na vizuri ikiwa tusingezungumza hata kidogo.
____ITAENDELEA____

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.